
TAMISEMI yazindua Awamu ya pili ya Mradi wa Green and Smart Cities unaoshirikisha Sekta Binafsi
Na OR -TAMISEMI, Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Vijiji na Miji kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Mkuki Hante, leo amezindua rasmi Mjadala wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi uliofanyika jijini Dar es Salaam, wenye lengo la kufungua miradi za uwekezaji kupitia ushirikiano kati ya Halmashauri na Sekta Binafsi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI Adolf Ndunguru, Dkt. Hante amesema Serikali imeandaa Rasimu ya Mpango wa Msaada wa Utekelezaji wa Miradi ya Halmashauri ili kuongeza ufanisi na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kipaumbele katika Halmashauri za Jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela na Jiji la Tanga.
“Tumeona changamoto nyingi katika maandalizi na utekelezaji wa miradi. Kupitia mpango huu tunataka kujenga uwezo wa Halmashauri, kuvutia wawekezaji na kuhakikisha miradi inatekelezeka kwa vitendo kupitia PPPs na ushirikiano mwingine wa Sekta Binafsi,” amesema
Mjadala huo ulihusisha viongozi wa Serikali za Mitaa, mabenki, taasisi za kifedha, mashirika ya hifadhi ya jamii, wawekezaji na washirika wa maendeleo ambapo washiriki walipata fursa ya kujadili miradi ya kipaumbele na kutoa ushauri juu ya namna ya kushirikiana katika utekelezaji.
Kwa mujibu wa Dkt. Hante, amesema Serikali imekubaliana kuanza na vipaumbele vitatu hadi vinne vya awali, ikiwemo mafunzo, ushauri wa kitaalamu na kujengea uwezo timu za Halmashauri.
“Mjadala huu si jukwaa la maneno pekee, bali ni daraja la kuunganisha nguvu kati ya sekta ya umma na binafsi kwa maendeleo ya wananchi,” amesisitiza Dkt. Hante.
Comments
Please sign in to leave a comment.