
TAMISEMI YAENDELEA KUIMARISHA UTENDAJI NGAZI YA MSINGI
Na OR-TAMISEMI, Katavi
Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeendeleza mafunzo elekezi kwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata wapya, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utendaji kazi katika ngazi ya msingi na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.
Mafunzo hayo yamefunguliwa leo Julai 28, 2025 mkoani Katavi na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bi. Florence Crisant, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI. Washiriki wa mafunzo wanatoka katika mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Bi. Crisant amesema Serikali inatambua nafasi muhimu ya Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata katika utekelezaji wa sera na maelekezo ya Serikali, hivyo mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji wa hali ya juu.
Amesema kuwa viongozi hao ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi, hivyo ni lazima wawe na uelewa sahihi wa sheria, kanuni na miongozo ya Serikali ili kuhakikisha utendaji kazi wao unaleta tija kwa taifa.
Kwa mujibu wa Crisant, mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kujenga viongozi wenye maadili, nidhamu na uwezo wa kusimamia rasilimali na miradi ya maendeleo kwa uwazi na ufanisi, pamoja na kuboresha mahusiano kati ya Serikali na wananchi.
Mafunzo haya yanatolewa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) na Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC), yakitekelezwa kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi unaohimiza utoaji wa mafunzo kwa watumishi wapya wa umma.
Aidha, katika kipindi cha mafunzo, washiriki wanatarajiwa kujengewa uelewa wa kina kuhusu muundo na majukumu yao ya kikazi, sera na sheria za Serikali, mbinu za kusimamia miradi ya maendeleo, namna ya kushughulikia kero za wananchi kwa wakati, pamoja na usimamizi bora wa rasilimali na mapato ya ndani.
Comments
Please sign in to leave a comment.
Matangazo Muhimu
Soma matangazo na taarifa rasmi ili kuendelea kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Wizara.
TANGAZO LA KUITWA KAZINI KWA WALIMU WA KUJITOLEA 128 SHULE ZA MSINGI 128 KWA AWAMU YA PILI GPE TSP
ORODHA YA WALIMU WA KUJITOLEA 128 GPE TSP AWAMU YA PILI
ADDITIONAL BEST INDICATORS 2025
BASIC EDUCATION STATISTICS 2025
Generic ESMP for CERC Interventions under DMDP2
Habari na Matukio
Soma matangazo na taarifa rasmi ili kuendelea kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Wizara.




