
SIDO YATOA MSUKUMO MPYA KATIKA MAENDELEO YA MJI WA TANGA KUPITIA MRADI WA INCLUCITIES
Na Angela Msimbira, Tanga
Maafisa waandamizi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI Tanzania Bara na Zanzibar, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wa kimataifa, wamefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Tanga kwa lengo la kujifunza na kufuatilia utekelezaji wa Mradi wa Green and Smart Cities unaotekelezwa kupitia programu ya IncluCities kwa usaidizi wa Enabel.
Katika ziara hiyo iliyofanyika Julai 2025, ujumbe huo ulijionea namna Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) linavyotoa mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya wakazi wa Jiji la Tanga, hasa wanawake na vijana, kupitia mafunzo ya ujuzi, ushauri wa kitaalamu, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya teknolojia vinavyowezesha uongezaji thamani wa bidhaa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mratibu wa Mradi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI Tanzania Bara, Bw. Shabani Ghuhia, amesema wamejionea kwa vitendo utekelezaji wa sera ya serikali ya kujenga miji jumuishi yenye uchumi shirikishi, kwa kupitia taasisi kama SIDO.
“SIDO imeonyesha mfano wa namna taasisi za ndani zinavyoweza kushirikiana na wadau wa kimataifa katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa kawaida. Huu ni mfano bora wa mafanikio ya ushirikiano wa maendeleo kati ya Serikali na mashirika ya kimataifa,” amesema Bw. Ghuhia.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji iliyowasilishwa kwa ujumbe huo, zaidi ya wajasiriamali 400 watanufaika na mafunzo ya kiufundi, ujasiriamali na matumizi ya teknolojia rafiki katika shughuli zao, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji, kupanua masoko ya bidhaa za ndani, na kuchochea matumizi ya mbinu bunifu zinazozingatia mazingira.
Aidha, ziara hiyo imekuwa jukwaa la kubadilishana uzoefu kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kuhusu utekelezaji wa sera na programu za maendeleo ya miji, pamoja na kutathmini namna bora ya kupanua miradi hiyo kwa mikoa mingine nchini.
Kwa upande wao, wawakilishi wa Enabel na programu ya IncluCities wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa dhamira yake madhubuti ya kujenga mifumo jumuishi ya maendeleo ya mijini, na kuahidi kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na mabadiliko ya kisera na kiuchumi yanayoendelea nchini.
Naye Mratibu wa Mradi wa Green and Smart Cities kutoka Pemba, Bi. Dhahira Mohamed Suleiman, amesema ziara hiyo imewasaidia kuelewa kwa kina namna mradi huo unavyotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Umoja wa Ulaya ambao ni wafadhili, pamoja na watekelezaji wake ambao ni Enabel, kwa kushirikiana na mashirika ya TRIAS, RIKOLTO, DOT, VETA na ENOVATE.
Amesisitiza kuwa ziara za namna hii zinapaswa kuwa endelevu ili kuwezesha ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa miradi na kuhakikisha malengo ya muda mrefu ya miji jumuishi na smart cities yanatimia kikamilifu.
Comments
Please sign in to leave a comment.
Matangazo Muhimu
Soma matangazo na taarifa rasmi ili kuendelea kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Wizara.
TANGAZO LA KUITWA KAZINI KWA WALIMU WA KUJITOLEA 128 SHULE ZA MSINGI 128 KWA AWAMU YA PILI GPE TSP
ORODHA YA WALIMU WA KUJITOLEA 128 GPE TSP AWAMU YA PILI
ADDITIONAL BEST INDICATORS 2025
BASIC EDUCATION STATISTICS 2025
Generic ESMP for CERC Interventions under DMDP2