
SERIKALI YASISITIZA KUDUMISHA AMANI NA USALAMA KUPITIA MAENDELEO SHIRIKISHI
Serikali imesisitiza umuhimu wa kuunganisha juhudi za maendeleo ya kijamii na kiuchumi kama nguzo muhimu ya kudumisha Amani na Usalama wa Nchi.
Akizungumza katika Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Duluti kilichopo Tengeru mkoani Arusha, Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba, akimuwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema kuwa juhudi za serikali za kuboresha huduma za jamii ni sehemu ya mikakati ya kudumisha utulivu na mshikamano wa kitaifa.
“Serikali haitachoka kuhakikisha huduma za afya, elimu na miundombinu zinawafikia wananchi wote kwani amani ya kudumu haiwezi kupatikana bila usawa katika upatikanaji wa huduma na fursa za maendeleo,” Amesema
Mhe. Katimba ameongeza kuwa serikali imeendelea kutekeleza sera na mikakati inayolenga kuondoa umasikini, ukosefu wa ajira na pengo la kijamii huku akisisitiza kuwa jitihada hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Miaka Mitano (2021/22–2025/26) na kusisitiza kuwa ushirikishwaji wa wananchi kupitia mfumo wa O&OD kuwa chachu ya kuongeza uwajibikaji na uhalisia katika miradi ya maendeleo.
Aidha, Mhe. Katimba alitoa wito kwa wadau wote wakiwemo sekta binafsi, mashirika ya kiraia na washirika wa maendeleo kushirikiana na serikali katika kuimarisha uchumi jumuishi unaojenga msingi wa amani, usawa na ustawi endelevu kwa taifa.
Comments
Please sign in to leave a comment.