
SERIKALI YAHIMIZA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA MALEZI NA MAKUZI YA AWALI YA MTOTO NCHI NZIMA
OR - TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Afya Prof. Tumaini Nagu, amewakumbusha na kuwataka Makatibu Tawala wa Mikoa, Maafisa Lishe na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanatekeleza kikamilifu Programu ya Kitaifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECDI 2030) ili kuwawezesha watoto kukua katika mazingira bora na kuzifikia ndoto zao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha uwasilishaji wa viashiria vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kilichofanyika leo Julai 2, 2025 Jijini Dodoma, Prof. Nagu amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa programu hiyo kuanzia ngazi ya Mkoa hadi ngazi ya jamii.
“Ndugu washiriki, natumia fursa hii kuwakumbusha kwenda kutekeleza kikamilifu programu hii ya kitaifa ili kuwawezesha watoto wetu kukua na kufikia utimilifu wao, ndoto zao zitimie na waweze kuwa na mchango mkubwa kwa taifa letu,” alisema Prof. Nagu.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa Mikoa na Halmashauri zote kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya kuchochea utekelezaji wa programu hiyo katika maeneo yao.
Awali, Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), Bwana Abbas Mtemba, alieleza kuwa kama Taifa bado kuna changamoto kubwa ya kuhakikisha watoto wote wanapata fursa sawa za ukuaji wa kiafya, kielimu, kiakili na kijamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (TECDEN), Bi. Mwajuma Kibwana, aliwasilisha takwimu za kitaifa zinazoonesha kuwa asilimia 47 pekee ya watoto wenye umri wa miezi 24 hadi 59 walio katika hatua ya ukuaji timilifu, huku asilimia 53 wakiwa bado wanakumbwa na changamoto mbalimbali katika malezi na makuzi yao.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makatibu Tawala wa Mikoa kutoka Mikoa 15, Maafisa Lishe wa Mikoa na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Comments
Please sign in to leave a comment.
Matangazo Muhimu
Soma matangazo na taarifa rasmi ili kuendelea kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Wizara.
TANGAZO LA KUITWA KAZINI WAOMBAJI WA NAFASI YA AJIRA YA MKATABA WA MAAFISA LISHE
CHAGUO LA PILI KIDATO CHA TANO
ORODHA YA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO WALIOPANGWA AWAMU YA PILI MWAKA, 2025
TANGAZO LA KUITWA KWENYE USAILI. (ORAL INTERVIEW)
Tangazo la kuitwa kazini ajira za TMCHIP 2025