
SERIKALI YAENDELEA KUWAJENGEA UWEZO VIONGOZI WA NGAZI ZA MSINGI
Na Hilary Shuma – OR-TAMISEMI
Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeendelea na jitihada zake za kuimarisha utendaji kazi wa viongozi wa Serikali ngazi ya msingi kwa kuwawezesha Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata wapya kupata mafunzo ya awali yanayolenga kuongeza ufanisi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza mapema leo Julai 25, 2025 katika ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bw. Rodrick Mpogolo, amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa kada hizo katika kufanikisha utekelezaji wa mipango na sera za Taifa kupitia ushirikiano wa karibu na wananchi katika maeneo yao ya kiutawala.
"Lengo letu ni kuwaandaa viongozi hawa kuanza kazi kwa misingi sahihi kwa kuwa wao ndio wawakilishi wa Serikali kwa wananchi katika maeneo yao ya utawala," amesisitiza Bw. Mpogolo.
Amebainisha kuwa mafunzo hayo yanalenga kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza katika utendaji wa viongozi wa ngazi ya msingi, zikiwemo migogoro ya mamlaka kati ya viongozi na wataalam, udhaifu katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, ucheleweshaji wa kutatua kero za wananchi, uelewa mdogo wa sera na sheria za Serikali pamoja na changamoto za kimaadili mahala pa kazi.
Bw. Mpogolo amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa viongozi wa mfano katika maeneo yao kwa kutumia maarifa, nidhamu na maadili katika kuwahudumia wananchi, huku wakisaidia kuchochea maendeleo katika jamii wanazoziongoza.
Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Waraka wa Utumishi Na. 5 wa mwaka 2011, unaozitaka taasisi za umma kuhakikisha kila mtumishi mpya anapatiwa mafunzo elekezi kabla ya kuanza kazi rasmi.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI, kwa kushirikiana na Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) na Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC), yakihusisha washiriki kutoka Mikoa ya Mbeya, Songwe, Ruvuma na Njombe.
Comments
Please sign in to leave a comment.
TANGAZO LA KUITWA KAZINI KWA WALIMU WA KUJITOLEA 128 SHULE ZA MSINGI 128 KWA AWAMU YA PILI GPE TSP
ORODHA YA WALIMU WA KUJITOLEA 128 GPE TSP AWAMU YA PILI
ADDITIONAL BEST INDICATORS 2025
BASIC EDUCATION STATISTICS 2025
Generic ESMP for CERC Interventions under DMDP2