
Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan yapongezwa kuunganisha nguvu na Wadau kuwapigania wasichana nchini
Mwenyekiti wa GPE Duniani, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete ameipongeza Serikali ya Tanzania chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada na hatua ilizofikia katika elimu kwa kuwezesha watoto wengi kuendelea na masomo, kuongeza ufaulu ngazi za sekondari ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu.
Mhe. Kikwete aliyasema hayo Kibasila sekondari Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kumkaribisha Mwanzilishi wa Mfuko wa Malala (Malala Fund) aliyekuja kwa mwaliko wa Kiongozi huyo. Kikwete amemtaja Malala kama shujaa wa kumpigania mtoto wa kike hususani wakati huu wa Sayansi na Teknolojia ambayo haitakiwi kumwacha nyuma mtoto yeyote.
Aidha, alisema Mfuko wa Elimu Duniani GPE umewezesha kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji wa wanafunzi na walimu kwa kujenga miundombinu ya madarasa 2980, vituo vya walimu (TRC) 252, uchapaji wa vitabu 36118000, matundu ya vyoo 7673, nyumba za walimu 64 na shule mpya 18 ambazo zimechangia kuleta mabadiliko nchini
Naibu Waziri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. QS Kipanga, alisema kuwa maboresho ya mitaala nchini yanalenga kuwahakikishia wanafunzi wote, hususan wasichana na wale wenye mahitaji maalum, mazingira salama na jumuishi ya kujifunzia yanayowasaidia kufanikisha malengo yao ikiwepo matumizi ya teknolojia za kidijitali, ikiwemo Akili Mnemba (AI) na TEHAMA
Vilevile, Mhe. Kipanga alisisitiza kuwa Serikali inaamini kuwa kumuelimisha mtoto wa kike ni njia ya msingi ya kulitendea haki Taifa kwa kulikomboa kiuchumi na kijamii lakini pia hadi sasa wanafunzi wapatao 13,272, wengi wao wakiwa wasichana, wamepata fursa ya pili ya kuendelea na elimu ya sekondari kupitia vituo vya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (IAE).
Bi. Malala Yousafzai, Mwanzilishi wa Mfuko wa Malala (Malala Fund), alisherehekea siku yake ya kuzaliwa tarehe 12 Julai, 2025, Wilayani Kongwa, Tanzania akieleza kufurahishwa na mazingira mazuri yanayoandaliwa kuwawezesha watoto wa Kitanzania kupata elimu. Malala alitoa wito kwa jamii na wadau kuungana kuwasaidia wasichana kutoka katika mazingira na historia tofauti ili wafikie ndoto zao. Alisema zaidi ya wasichana milioni mbili nchini Tanzania wanakosa fursa ya kuendelea na masomo, huku theluthi moja yao wakikatishwa masomo yao na kuolewa mapema. Malala alisisitiza kuwa jambo hili ni hasara kwa Taifa kiuchumi, na kuwa Serikali ikishirikiana na jamii wana uwezo wa kuhakikisha wasichana wote wanahitimu elimu yao.
Joyline Buntu, mwanafunzi wa Kidato cha Pili kutoka Shule ya Sekondari Kibasila, ameishukuru Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Programu ya GPE na Taasisi ya Jakaya Kikwete kwa kuunganisha nguvu pamoja na kuwezesha wanafunzi kama yeye kubaki shuleni, kujifunza kwa ufanisi, pia kujenga miundombinu bora na kufikia ndoto zao bila kukumbana na vikwazo vyovyote.
Malala Yousafzai, Mwanzilishi wa mfuko wa Malala alitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kujionea moja ya Taasisi ambayo inatekeleza jukumu la kuwainua wasichana waliorudi shule baada ya kuanguka (school dropout) la ‘Msichana Initive’ lakini pia kuunga mkono jitihada za kuwawezesha wasichana nchini ambapo anatarajiwa kuwekeza kiasi cha shilingi Bilioni 8 mwaka 2026.
Comments
Please sign in to leave a comment.
Matangazo Muhimu
Soma matangazo na taarifa rasmi ili kuendelea kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Wizara.
TANGAZO LA KUITWA KAZINI WAOMBAJI WA NAFASI YA AJIRA YA MKATABA WA MAAFISA LISHE
CHAGUO LA PILI KIDATO CHA TANO
ORODHA YA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO WALIOPANGWA AWAMU YA PILI MWAKA, 2025
TANGAZO LA KUITWA KWENYE USAILI. (ORAL INTERVIEW)
Tangazo la kuitwa kazini ajira za TMCHIP 2025