
Serikali kujenga hospitali mpya 43 za kisasa
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Festo Dugange amesema serikali itajenga hospitali 43 za halmashauri katika mwaka huu wa fedha ili kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za afya nchini
Dkt. Dugange amesema hayo wakati akifunga kikao kazi cha Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri Tanzania Bara, kilichofanyika kwa siku 3 jijini Dodoma kuanzia tarehe 11 hadi 13 julai, 2025.
Mhe. Dugange amesema ujenzi wa hospitali hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati madhubuti na ya kimkakati ya maendeleo kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Ujenzi wa Hospitali 43 za Halmashauri umelenga kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za afya kwa wananchi walioko pembezoni mwa Miji,” Dkt. Dugange amesisitiza.
Sanjari na ujenzi wa hospitali hizo, Dkt. Dugange amesema Serikali itanunua vifaa tiba kwa ajili ya hospitali 142, vituo vya afya 184, pamoja na zahanati 184 ambazo zitakarabatiwa au kujengwa katika Mwaka wa Fedha 2025/2026.
Amefafanua kuwa, hatua hizi zinadhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma za afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Aidha amewataka Waganga Wakuu hao wakaimarishe ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi katika vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoko kwenye maeneo yao ya usimamizi.
Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Dugange, Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI (Afya) Prof. Tumaini Nagu amesema kikao kazi hicho kimetoa fursa ya kujadili na kuweka mikakati ya kuboresha huduma za afya msingi kwa wananchi ili wanufaike na uwekezaji wa trilioni 1.28 uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujenga miundombinu ya afya msingi pamoja na ununuzi wa vifaa tiba.
Comments
Please sign in to leave a comment.