
SERIKALI IMEDHAMIRIA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI – PROF. NAGU
OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Prof. Tumaini Nagu, amesema kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazowakabili wananchi, hususan katika sekta ya afya.
Prof. Nagu ametoa kauli hiyo alipotembelea mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Muhoro, kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Rufiji, mkoani Pwani, ambacho kimekuwa kikikumbwa na tatizo la mafuriko ya mara kwa mara.
> “Kituo chetu cha sasa cha Muhoro kimekuwa na changamoto ya mafuriko kila mara. Ili kukabiliana na hali hiyo, Serikali imeamua kujenga kituo kipya katika eneo ambalo halifikiwi na maji kwa urahisi. Hii ni hatua ya kutoa suluhisho la kudumu kwa wananchi wa Kata ya Muhoro na maeneo ya jirani,” alisema Prof. Nagu.
Aliongeza kuwa Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 700 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho, ambacho kinatarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.
Aidha, Prof. Nagu amewataka watumishi wa afya wa kituo hicho kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi mara tu kituo kitakapokamilika, kama ilivyo dhamira ya Serikali ya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi na weledi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Rufiji, Bw. Simon Berege, amesema kukamilika kwa kituo hicho kutakuwa ni msaada mkubwa si kwa wakazi wa Kata ya Muhoro pekee, bali pia kwa wananchi kutoka maeneo mengine ya halmashauri hiyo, pamoja na baadhi ya wananchi kutoka mkoa jirani wa Lindi.
Comments
Please sign in to leave a comment.