
MRADI WA INCLUCITIES WAIBUA MAGEUZI KWENYE MIFUMO YA CHAKULA NA BIASHARA JIJI LA TANGA
Na Angela Msimbira, Tanga
Mradi wa IncluCities unaotekelezwa katika Jiji la Tanga kwa ushirikiano kati ya Halmashauri ya Jiji hilo na shirika la kimataifa la Rikolto, umeleta mageuzi makubwa katika kuboresha mifumo ya chakula, kuwawezesha wakulima wadogo na kuhamasisha biashara jumuishi miongoni mwa wanawake na vijana.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi huo, Eliud Ng'umbi, Mshauri wa Programu kutoka Rikolto, amesema kuwa utekelezaji wa IncluCities umeongeza tija kwa wakulima na wajasiliamali kupitia elimu, teknolojia rafiki kwa mazingira na urasimishaji wa biashara ndogondogo.
"Tumeanzisha jukwaa la Tanga Sustainable Food Systems (TSFS) lenye makundi manne ya kazi, likiwa ni jukwaa shirikishi kwa wadau mbalimbali wanaojihusisha na mnyororo wa thamani wa chakula na kuunda vikundi vitano vya biashara ya kilimo vinavyowaleta pamoja wakulima 727, ambapo wanawake ni zaidi ya 300,” amesema Ng’umbi.
Anafafanua zaidi kuwa mradi huo pia umewezesha mashamba ya mfano kuanzishwa katika kila kikundi, ambapo wakulima wamepata mafunzo juu ya matumizi ya mbegu bora, umwagiliaji kwa kutumia nishati ya jua na utengenezaji wa mashamba darasa.
Vilevile, amesema kuwa katika kuimarisha mazingira rafiki kwa biashara ndogondogo, mradi wa IncluCities kupitia Shirika la Rikolto uliandaa Kliniki ya urasimishaji biashara kwa kushirikiana na taasisi kama TRA, BRELA, TBS na SIDO ambapo kliniki hiyo iliwezesha zaidi ya wajasiriamali 100 kupata elimu ya mabadiliko kutoka sekta isiyo rasmi kwenda rasmi, ambapo tayari wajasiriamali 16 wameanza mchakato wa usajili rasmi.
"Tunashirikiana na SIDO kufanya tathmini ya programu ya kukuza biashara kwa vijana na wanawake, sambamba na kuandaa kanzidata ya kisasa ya wanachama wa TCCIA na TWCC kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa taarifa na huduma,” ameongeza Ng’umbi.
Amesema katika hatua nyingine, kanzidata ya wakusanyaji wa taka za chakula inaandaliwa kwa ajili ya kushirikishwa katika mfumo wa uchakataji wa taka kwa matumizi ya kilimo.
"Mradi pia unaendelea kuwajengea uwezo wakulima kuhusu matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira na usimamizi endelevu wa rasilimali.", amesema
Mradi wa IncluCities, unaoratibiwa kimataifa na Baraza la Miji na Majiji ya Ulaya (CEMR), unalenga kuleta mabadiliko ya kweli katika utawala jumuishi wa miji, huku ukizingatia usawa wa kijinsia, ujumuishaji wa vijana, na maendeleo endelevu.
Kwa Jiji la Tanga, mafanikio haya ni ishara ya utayari wa kutumia fursa za kimataifa kuboresha maisha ya wakazi na mazingira ya kiuchumi kwa njia shirikishi na endelevu.
Mradi huu umekuwa chachu ya maendeleo kwa kina mama na vijana kuongeza kipato lakini pia umesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira. Kama unavyojua, dunia kwa sasa inapambana kuhakikisha mazingira yanatunzwa na kuwa sehemu salama.
Comments
Please sign in to leave a comment.
TANGAZO LA KUITWA KAZINI KWA WALIMU WA KUJITOLEA 128 SHULE ZA MSINGI 128 KWA AWAMU YA PILI GPE TSP
ORODHA YA WALIMU WA KUJITOLEA 128 GPE TSP AWAMU YA PILI
ADDITIONAL BEST INDICATORS 2025
BASIC EDUCATION STATISTICS 2025
Generic ESMP for CERC Interventions under DMDP2