
Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata waaswa kutochagua mazingira ya kufanyia kazi.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Daniel Machunda ametoa wito kwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kutochagua Mazingira ya kufanyia kazi kwani wananchi walio katika vituo vyao vya kazi walivyopangiwa wanastahili kupata huduma bora kama wanazopata watanzania wengine walio katika maeneo ya miji.
Bw. Machunda ametoa rai hiyo jijini Mwanza, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Geita na Kagera.
Bw. Machunda amewasisitiza Maafisa Tarafa na Watendaji Kata hao kuzingatia weledi, maadili, kanuni, miongozo na taratibu za Utumishi wa Umma ili waweze kutoa huduma bora zisizo na mlengo wa ubaguzi.
Aidha, Bw. Machunda amewataka maafisa hao kuwa mstari wa mbele kuisemea Serikali pale inapobidi, kwa kuanisha kazi kubwa ya utekelezaji miradi ya maendeleo iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika maeneo yao ya kiutawala.
“Siyo sawa mtumishi wa serikali kukaa kimya wakati Serikali unayoitumikia inachafuliwa kwa taarifa za uongo ilihali ukifahamu fika serikali imefanya nini katika hicho kinachozungumziwa, nendeni mkawe sauti ya Serikali kwa wananchi” alisisitiza Bw. Machunda.
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inaendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji waajiriwa wapya wa kada za Maafisa Tarafa na Watendaji wa kata ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Comments
Please sign in to leave a comment.