
Dkt. Jakaya Kikwete: Elimu ni Silaha Dhidi ya Changamoto za Dunia
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema kuwa elimu ni silaha muhimu ya kupambana na changamoto mbalimbali za dunia ya sasa. Amewahimiza wadau wa elimu kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha kila mtoto, bila kujali mazingira yake, anapata haki yake ya msingi ya kupata elimu.
Akizungumza Dar es Salaam, Julai 13 katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa kitaifa, wadau wa elimu na mashirika ya kimataifa, Dkt. Kikwete alisisitiza kuwa licha ya hatua kubwa zilizofikiwa katika kupanua fursa za elimu, bado kuna uhitaji mkubwa wa kusaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu ili waweze kutimiza ndoto zao.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alieleza kuwa hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma katika safari ya elimu. Alibainisha kuwa uwekezaji katika elimu ya mtoto wa kike ni msingi wa maendeleo ya kijamii na ya taifa kwa ujumla. Prof. Mkenda alisema msichana anapopewa elimu, jamii nzima inanufaika kiuchumi, kijamii na kiafya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Malala Fund, Lena Alfi, naye alieleza kuwa taasisi hiyo imejipanga kushirikiana kwa karibu na serikali ya Tanzania pamoja na wadau wa ndani kwa lengo la kuleta mageuzi ya kweli katika elimu ya mtoto wa kike.
Aidha, tarehe 14 Julai, 2025, wajumbe wa kimataifa kutoka mashirika hayo wanatarajiwa kutembelea shule mbalimbali jijini Dar es Salaam. Ziara hiyo imelenga kukagua hali halisi ya miundombinu ya shule na kujionea jinsi ambavyo serikali pamoja na wadau wa elimu wamewekeza katika kuboresha mazingira ya kujifunzia. Pia, ziara hiyo itasaidia kubaini maeneo yanayohitaji uboreshaji wa haraka ili kuwezesha elimu bora kwa wote.
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF), Malala Fund, na Global Partnership for Education (GPE)
Comments
Please sign in to leave a comment.
TANGAZO LA KUITWA KAZINI KWA WALIMU WA KUJITOLEA 128 SHULE ZA MSINGI 128 KWA AWAMU YA PILI GPE TSP
ORODHA YA WALIMU WA KUJITOLEA 128 GPE TSP AWAMU YA PILI
ADDITIONAL BEST INDICATORS 2025
BASIC EDUCATION STATISTICS 2025
Generic ESMP for CERC Interventions under DMDP2