
BOOST YALETA MAGEUZI ELIMU YA MSINGI, UJENZI WA MADARASA ZAIDI YA 15,000 WASHAMIRI NCHI NZIMA
Na. Angela Msimbira, MOROGORO
Mratibu wa Mradi wa BOOST kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ally Swalehe amesema Programu ya BOOST imeendelea kuleta matokeo makubwa katika kuboresha elimu ya awali na msingi tangu kuanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2021/2022, huku ikitarajiwa kukamilika mwaka 2026/2027.
Amesema lengo kuu la programu ni kuboresha ujifunzaji wa Elimu ya Awali na Msingi kupitia meneo makuu matatu, kuimarisha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji, umahiri na utendaji wa walimu darasani, na uzingatiaji wa vigezo vya utawala bora.
Ameeleza kuwa thamani ya programu ni shilingi trilioni 1.12, sawa na dola milioni 500 za Kimarekani, ambapo asilimia 96 ya fedha hutolewa kupitia mfumo wa “lipa kulingana na matokeo” na asilimia 4 hupitia utaratibu wa kugharamia miradi moja kwa moja. Programu hii inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambapo Wizara ya Elimu hutoa miongozo na viwango, huku TAMISEMI ikiratibu na kusimamia utekelezaji katika ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Akitoa ufafanuzi kuhusu maeneo ya utekelezaji, Swalehe alisema mradi wa BOOST una afua saba, zikiwamo kuboresha miundombinu ya shule. Katika eneo hilo, lengo lilikuwa kujenga vyumba 12,000 vya madarasa sambamba na miundombinu ya usafi na maji, lakini hadi sasa zaidi ya vyumba 15,000 vimejengwa na vingine vinaendelea kukamilika katika shule za awali, msingi na sekondari ili kuwezesha utekelezaji wa Elimu ya lazima ya Miaka 10.
Aidha, kupitia Mpango wa Shule Salama, BOOST imelenga kuimarisha usalama wa wanafunzi ili kuhakikisha wanamaliza mzunguko wa elimu bila changamoto. Lengo lilikuwa kufikia shule 6,000, lakini kwa sasa shule zote za awali na msingi zilizolengwa zimefikiwa, huku walimu na viongozi wakijengewa uwezo katika utekelezaji wa afua hizo.
Katika kuongeza uandikishaji wa elimu ya awali (Gross Enrollment Ratio), lengo la mradi lilikuwa kufikia asilimia 85 mwaka kutoka asilimia 76.9 ya mwaka 2021, na hadi kufikia mwaka 2024 kiwango hicho kimepanda hadi asilimia 89. Swalehe pia alieleza kuwa mradi umeimarisha umahiri wa walimu kupita mafunzo maalum ya mbinu bora za ufundishaji, aidha, shule 12,302 zimewezeshwa kununua na kuandaa vifaa vya kujifunzia na kufundishia Elimu ya Awali.
Ameongeza kuwa, mwaka 2024, vifaa vya TEHAMA vilinunuliwa na kusambazwa katika shule za msingi 200 na mwaka huu 2025 vimenunulliwa vifaa vya TEHAMA na usambazaji umeanza katika shule 600 ili kuwezesha matumizi ya stadi za digiti katika ufundishaji na ujifunzaji.
Swalehe amehimiza kwa kusema kuwa mafanikio yanayoonekana kupitia utekelezaji wa BOOST ni ushahidi thabiti wa dhamira ya Serikali kuboresha elimu ya msingi nchini, na kujenga msingi imara kwa kizazi kijacho chenye ujuzi, umakini na nidhamu ya kielimu.
Comments
Please sign in to leave a comment.
TANGAZO LA KUITWA KAZINI KWA WALIMU WA KUJITOLEA 128 SHULE ZA MSINGI 128 KWA AWAMU YA PILI GPE TSP
ORODHA YA WALIMU WA KUJITOLEA 128 GPE TSP AWAMU YA PILI
ADDITIONAL BEST INDICATORS 2025
BASIC EDUCATION STATISTICS 2025
Generic ESMP for CERC Interventions under DMDP2