
BIL. 1.9/- ZABORESHA HUDUMA ZA AFYA HANDENI MJI
Na Mwandishi Wetu, Handeni
Halmashauri ya Mji wa Handeni mkoani Tanga imenufaika na zaidi ya Sh. bilioni 1.9 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kuboresha huduma za afya, ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya kisasa katika Hospitali ya Halmashauri hiyo.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa miradi ya kimkakati, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Maryam Ukwaju, amesema fedha hizo zimetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na zimetumika kujenga jengo la wagonjwa mahututi (ICU), chumba cha kuhifadhi maiti na maabara ya kisasa.
Ukwaju amesema uboreshaji huo utasaidia kwa kiwango kikubwa kuinua huduma za afya kwa wananchi wa mji huo na maeneo jirani.
“Majengo hayo tayari yamekamilika na yanakwenda kuongeza ufanisi katika kutoa huduma bora za afya. Pia tumepokea fedha nyingine kwa ajili ya ukarabati wa baadhi ya majengo ya zamani,” amesema Ukwaju.
Aidha, ametoa pongezi kwa Serikali kwa kuendelea kuwekeza kwenye Sekta ya Afya ambayo ni miongoni mwa maeneo ya kipaumbele ya maendeleo ya wananchi.
Comments
Please sign in to leave a comment.